Joy FM
Joy FM
14 July 2026, 15:25

Wazee ni hazina ya taifa na msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na wametumia nguvu, maarifa na uzoefu wao katika kujenga taifa na kulea vizazi mbalimbali kutokana na mchango wao mkubwa, serikali ina wajibu wa kuhakikisha wanapata huduma na ulinzi unaostahili ili waishi maisha yenye heshima na ustawi
Na Lucas Hoha
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya maisha ya wazee wasiojiweza nchini kupitia utoaji wa bima ya afya na uboreshaji wa miundombinu ya makazi yao ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wa wazee kwenye jamii.
Akizungumza baada ya kutembelea Kituo cha Makazi ya Wazee Wasiojiweza cha Silabu kilichopo Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema wazee wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa kwa kuwa wameendelea kuwa nguzo muhimu katika jamii.
Awali, Afisa Ustawi wa Jamii na Msimamizi wa Makazi ya Wazee wasiojiweza Silabu, Binura Abbas Joshua, amesema kituo hicho kinaendelea kuwahudumia wazee kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo, wakiwemo shirika la Joy in The Harvest, ambao wamekuwa wakichangia huduma mbalimbali kwa ustawi wa wazee hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, ameipongeza Serikali kwa juhudi zinazoendelea kufanyika katika kuwahudumia wazee wasiojiweza, ikiwemo kuwawezesha kupata huduma za afya, chakula na mavazi.

Kituo cha kulea na kutunza wazee wasiojiweza cha SILABU Kilichopo Manispaa ya Kigoma Ujiji kina jumla ya wazee 22 wanawake wakiwa 10 na wanaume wakiwa ni 12