Joy FM
Joy FM
29 June 2026, 08:21

Elimu kuhusu ukatili ni sehemu muhimu ya kulinda usalama, afya, na ustawi wa watoto na inapaswa kutolewa kwa lugha na mbinu zinazolingana na umri wa mtoto kwa mazingira yanayowafanya wajisikie salama kuuliza maswali na kutoa taarifa wanapohitaji msaada
Na Mwandishi wetu
Shirika la World Vision limeendelea kuimarisha juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto kwa kutoa elimu ya ulinzi na Usalama wa mtoto kwa makundi mbalimbali ya jamii Wilayani Kakonko.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Africa yaliyofanyika kiwilaya katika Kata ya Gwarama mwakilishi wa shirika la world Vision Isack Eliah, Ameeleza kuwa ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika na familia dunia shirika limefanikiwa kufikia makundi mbalimbali yakiwemo mabaraza ya watoto,kamati za mtakuwa, waendesha bodaboda, kago pamoja na viongozi wa dini kwa kuwapatia Elimu inayolenga kuongeza uelewa kuhusu ulinzi wa mtoto na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aidha ameeleza Shirika hilo litaendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kulinda watoto na kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia pamoja na kuhamasisha malezi bora na utetezi wa haki za mtoto.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Abdallah Mwamachi amepongeza juhudi zinazofanywa na shirika la World Vision katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ulinzi wa mtoto ambapo ameeleza kuwa elimu inayotolewa imekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha wananchi na kutambua na kuripoti matukio ya ukatili wa kijijnsia jambo linalosaidia kulinda haki na ustawi wa mtoto.
Aidha ameeleza kuwa mafanikio ya kupambana na ukatili wa kijinsia yanategemea ushirikiano wa wadau wote hivyo ameitaka jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na badala yake watoe taarifa pindi vitendo hivyo vinapotokea katika jamii na kuhakikisha watoto wanalindwa wakati wote.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mustapha Mtungwe, ameeleza kuwa ushirikiano kati ya wadau wa maendeleo umeendelea kuleta matokeo chanya katika juhudi za kulinda watoto huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama wakati wote.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki na ulinzi unaohitajika.
