Joy FM

Serikali yatoa msaada kwa waathirika wa mafuriko Katubuka

5 May 2025, 13:01

Muonekano wa maji yalijaa katika makazi ya watu katika eneo la Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji, Picha na Emmanuel Senny

Serikali imekabidhi msaada wa vitumbalimbali kwa waathirika wa mafuriko eneo la Katubuka Manispaa ya Kiagoma Ujiji.

Na Emmanuel Senny

Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya waathirika waliokumbwa na kadhia ya mafuriko katika eneo la Katubuka lililopo kata ya Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji  mkoani Kigoma.

Mara baada ya kupokea misaada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu huku akisisitiza kuwa pamoja na misaada hiyo, serikali ilishapeleka wataalam katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuja na suluhisho la kudumu dhidi ya kadhia hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akipokea msaada wa waathirika wa mafuriko kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Picha na Emmanuel Senny

Amesema Serikali imeendelea kufuatilia kwa karibu na kutoa  makatazo kwa jamii kutoendelea kuishi katika eneo hilo pamoja na kuhakikisha waathiriwa na wakazi katika maeneo jirani wanaendelea kuwa salama.

Kirumbe Ng’enda Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini amesema serikali imefanya jambo la kiutu na kuthibitisha kuwa  ni sikivu na yenye kujali wananchi wake.

Amesema katika kupata suluhu ya kudumu ya changamoto ya kujaa maji katika eneo hilo, serikali ipo katika hatua za uchunguzi ili iweze kuandaa mpango utakaoleta suluhisho la kudumu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua amesema ameipokea misaada hiyo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na atahakikisha inawafikia wananchi kama ilivyopangwa.

Upande wake Mkurugenzi anayeshugulikia Operesheni na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Celestine Masalamado amesema misaada hiyo imekuja kufuatia ombi la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma lililolenga  kuongezewa nguvu katika kusaidia kukabiliana na changamoto za wakazi walioathiriwa na mafuriko katika eneo hilo.

Ameitaja misaada iliyotolewa kuwa ni pamoja na Mahindi tani 15.6, Maharage tani 4.6, magodoro 283, Blanket 283, ndoo 283, mikeka 283 ambapo jumla ya kaya 283 zenye wakazi 1304 zitanufaika katika kata za Katubuka, Kibirizi na Bangwe.

Msaada wa vitu vilivyotolewa kwa waathirika wa mafuriko, Picha na Emmanuel Senny