Joy FM
Joy FM
22 May 2026, 10:30

Maonesho ya biashara ni mikusanyiko inayowakutanisha wafanyabiashara, wazalishaji, wanunuzi na wananchi kwa lengo la kuonyesha bidhaa na huduma mbalimbali
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amezitaka mamlaka za kibiashara za Tanzania na Burundi kushughulikia changamoto ya vikwazo visivyo vya kikodi ili kuimarisha Biashara baina ya mataifa hayo mawili.
Balozi Sirro ametoa wito huo alipomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara kwenye ufunguzi wa maonesho ya pamoja ya biashara baina ya Tanzania na Burundi Mei 22, 2026, yanayofanyika jijini Bujumbura nchini Burundi.

Amesema pande zote mbili zinapaswa kushughulikia vikwazo hivyo ikiwemo uratibu wa kibiashara, taratibu zinazochukua muda mrefu kibiashara, utoaji wa maamuzi ya busara bila kuzingatia kanuni na Sheria pamoja na kuharakisha utekelezaji taratibu za kimipaka ili kurahisisha ukuaji wa kiwango cha Biashara.
Upande wake Balozi wa Tanzania nchini Burundi Gelasius Byakanwa amesema maonesho hayo yamelenga kutanua wigo wa masoko na kupata wateja wapya.

Amesema maonesho yanatumika kama jukwaa jipya la kutangaza fursa na kupata wawekezaji wapya kwa pande zote mbili kwendana na mahitaji ya kibiashara.
Naye Josias Bigirimana ambaye ni mfanyabiashara katika jiji la Burundi amesema maonesho hayo ya pamoja, yamewapa fursa ya kubadilishana ujuzi na taarifa za kimasoko baina yao na wafanyabiashara wa Tanzania.

“Tumekutana hapa tunabadilishana taarifa za kibiashara hii inatupa nafasi kujua ni wapi na kwa kiwango Gani wenzetu wamefanikiwa lakini pia wao kufahamu pia mafanikio yetu pamoja na fursa zilizopo” amesema Bigirimana