Joy FM
Joy FM
3 June 2026, 14:11

Malezi bora ya watoto ni msingi muhimu wa kujenga familia imara na taifa lenye maendeleo endelevu na kutokana na kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto, ikiwemo ulawiti, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, kampeni ya malezi, makuzi na matunzo ya Mtoto imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu wajibu wa kumlinda na kumlea mtoto katika mazingira salama
Na Filbert Gabriel
Jamii ya Mkoa wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kuunganisha nguvu za pamoja katika kutoa malezi chanya kwa watoto ili kukomesha matukio ya ukatili dhidi ya watoto yanayoendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Mkoa ya Malezi, Makuzi na Matunzo ya Mtoto, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma, Msafiri Nzunuri, alisema kwa sasa kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili, hususan ulawiti mashuleni, jambo linalozua maswali kuhusu mazingira yanayochangia watoto kujifunza tabia hizo.

Alieleza kuwa ukosefu wa mawasiliano mazuri kati ya wazazi na watoto, ukuaji wa teknolojia bila uangalizi wa kutosha pamoja na ubinafsi katika jamii ni miongoni mwa sababu zinazochochea matukio hayo. Alibainisha kuwa mara nyingi waathirika wakuu wa vitendo hivyo ni watoto wa kiume, ambao ni baba wa baadaye na nguzo muhimu ya jamii.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma, Mwalimu Paulina Ndigeza, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, alisema kuwa ukosefu wa elimu na baadhi ya imani potofu za kishirikina ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kupigwa vita kwa nguvu zote. Alisema baadhi ya watoto waliobainika kuhusika au kuathirika na vitendo vya ulawiti walieleza kuwa walijifunza tabia hizo kutoka katika mazingira ya nyumbani.

Alisisitiza kuwa kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo, kuna haja kwa kila mzazi, mlezi, kiongozi wa jamii na wa dini kuhakikisha wanazungumza kwa uwazi na watoto kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya ukatili wa kijinsia na madhara yanayotokana na vitendo hivyo.
Kampeni ya Malezi, Makuzi na Matunzo ya Mtoto itatekelezwa kwa kipindi cha mwezi mmoja ikiwa na kaulimbiu isemayo: “Mtoto ni Malezi: Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara.”