Joy FM

Watumishi wa umma watakiwa kufanya kazi kwa weledi Kasulu

7 May 2026, 09:05

Baadhi ya watumishi wakiwa katika kikao hicho, Picha na Mwandishi wetu

Katibu tawala Wilaya ya Kasulu BI. Therezia Mtewele amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa biidi na weledi na mshikamano katika kuwahudumia wananchi ili kuweza kufanikisha mipango ya kuwahudumia wananchi

Na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma imefanya kikao cha uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya kata kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, kikiangazia mafanikio na changamoto mbalimbali katika kuwahudumia wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Teresia Mtewele, amesisitiza umuhimu wa watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mheshimiwa Ayubu Ngalaba Kilugu, ametoa wito kwa viongozi na watendaji mbalimbali ambao sekta zao zimeonekana kulalamikiwa mara kwa mara katika taarifa za kata kujitathmini ili kupunguza changamoto hizo, huku akiwaomba wataalamu kutumia utaalamu wao kikamilifu kwa kuwa rasilimali na vifaa vinavyohitajika vipo, hivyo hakuna sababu ya matatizo kuendelea kujirudia.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mwalimu Vumilia Simbeye, ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika robo hiyo yametokana na ushirikiano wa kiwango cha juu uliopo, huku akihimiza kuwepo kwa mshikamano dhabiti zaidi ili kutatua changamoto zilizobainishwa, hususan zile zilizo ndani ya uwezo wa utendaji wa ngazi za chini.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mwalimu Vumilia Simbeye, Picha na Mwandishi wetu