Joy FM
Joy FM
18 June 2026, 09:50

Chuo cha Veta Kigoma kimeendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na ukatili kwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi kupitia dawati la jinsia lililoanzishwa chuoni hapo
Na Timotheo Leonard
Ukatili wa kijinsia unaendelea kuwa changamoto kubwa katika jamii, hali inayochochea juhudi za wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata elimu na msaada wa kukabiliana na vitendo hivyo.
Katika juhudi hizo, Dawati la Jinsia lililoanzishwa katika VETA Kigoma mwezi Julai 2025 linaelezwa kuleta mafanikio ya awali kwa wanafunzi pamoja na jamii inayozunguka chuo hicho.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wamesema uwepo wa dawati hilo umewaongezea uelewa kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na namna ya kujikinga dhidi ya vitendo hivyo.
Mratibu wa Dawati la Jinsia la Kupinga Ukatili katika chuo hicho, Eunice John Masika, amesema mwitikio wa wanafunzi na wananchi katika kutumia huduma za dawati hilo umeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu kuanzishwa kwake.

Amesema dawati hilo limekuwa sehemu salama ya kupata ushauri, elimu na msaada kwa wanafunzi na wanajamii wanaokumbana na changamoto zinazohusiana na ukatili wa kijinsia.
Takwimu za chuo zinaonesha kuwa VETA Kigoma ina wanafunzi 529 wa kozi za muda mrefu, huku zaidi ya wanafunzi 1,000 wakishiriki kozi mbalimbali za muda mfupi.
Mkuu wa Chuo cha VETA Kigoma, Paul Kimenya, amesema Dawati la Jinsia lilianzishwa kwa lengo la kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, kuhamasisha utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili na kusaidia wahanga kupata huduma stahiki.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii, Binura Joshua, amesema uwepo wa madawati ya jinsia katika taasisi za elimu ni hatua muhimu katika kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Wadau mbalimbali wanaamini kuwa kuimarika kwa huduma za Dawati la Jinsia katika VETA Kigoma kutachangia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia, kuhamasisha utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili na kujenga kizazi cha vijana kitakachokuwa mabalozi wa kupinga ukatili katika jamii.