Joy FM

Mradi wa uhimilivu mabadiliko tabianchi waanzishwa Kibondo

28 April 2026, 10:18

Baadhi ya viongozi na wananchi mara baada ya kikao cha kujadili mrdai wa mabadiliko ya tabianchi, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kibondo

Elimu ya mabadiliko ya tabianchi si tu kuongeza maarifa, bali ni chombo muhimu cha kuboresha maisha, kulinda mazingira, na kuhakikisha maendeleo endelevu

Na Mwandishi wetu

Mfuko wa Green Climate Fund (GCF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais imeanzisha mradi muhimu wa kuimarisha uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika Wilaya ya Kibondo, ukiwa na lengo kuu la kuwasaidia makundi yaliyo hatarini zaidi, hususan wananchi wasio na kipato cha uhakika.

Mradi huu unakuja katika wakati muafaka ambapo athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, mabadiliko ya mifumo ya mvua, na upungufu wa rasilimali muhimu zinaendelea kuathiri maisha ya watu wengi vijijini.

Wananchi wakiwa katika kikao cha utekelezaji wa mradi, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kibondo

Katika utekelezaji wake, timu ya wataalamu kutoka UNEP na Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI ) walitembelea vijiji viwili, ambavyo ni Kifura na Nyaruyoba, kwa lengo la kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kuhusu malengo, mikakati na manufaa ya mradi huo.

Wananchi wa vijiji hivyo walipata fursa ya kushiriki katika mkutano ya hadhara ambapo walielezwa jinsi watakavyonufaika na programu mbalimbali zitakazotekelezwa chini ya mradi huo.

Miongoni mwa vipengele muhimu vya mradi ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbinu bora za kilimo himilivu, Kilimo cha Mseto, Ufugaji wa Nyuki, Hati za kimila, Usimamizi wa Misitu ya Jamii pamoja na uanzishaji wa shughuli mbadala za kiuchumi zitakazosaidia kuongeza kipato kwa kaya maskini.

Elimu ya mradi wa uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi ikitolewa kwa wananchi Kibondo, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kibondo

Aidha, mradi unalenga kujenga uelewa mpana kwa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na namna bora ya kujikinga dhidi yake kwa kutumia maarifa ya kisasa na ya jadi.

Wananchi wa Kifura na Nyaruyoba walionyesha mwitikio chanya na matumaini makubwa kuhusu mradi huo wakieleza kuwa utasaidia kuboresha hali zao za maisha na kupunguza utegemezi kwa vyanzo visivyo endelevu vya kipato.

Viongozi wa vijiji hivyo pia walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha mafanikio ya mradi huo.