Joy FM
Joy FM
27 May 2026, 12:42

Mradi wa kugeuza taka kuwa fursa ya kiuchumi una mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwani unasaidia kuongeza kipato, kulinda mazingira, kuboresha usafi pamoja na kuhamasisha matumizi bora ya taka
Na Lucas Hoha
Shirika la Catholic Relief Services (CRS) kwa kushirikiana na Caritas pamoja na wadau wengine wakiwemo shirika la JIDI, chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya, wametoa mafunzo kwa wananchi wa Wilaya ya Kigoma hususan wanawake na vijana kuhusu namna ya kugeuza taka kuwa fursa ya kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya wananchi kutoka Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutambua umuhimu wa taka na namna zinavyoweza kuwanufaisha kiuchumi tofauti na walivyokuwa wakiamini hapo awali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Afisa Usafi na Udhibiti wa Taka kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Innocent Mdunya, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha utunzaji wa mazingira pamoja na kupunguza uchafu unaoingia katika Ziwa Tanganyika.

Kwa upande wake, Msemaji wa Shirika la Jamii Integrated Development Initiative (JIDI) lenye makao makuu Jijini Dar es Salaam, Issack Kitururu, amesema kampeni ya “Taka ni Pesa” inalenga kubadili mtazamo wa wananchi ili waone taka kama fursa ya maendeleo ya kiuchumi badala ya uchafu.
Mradi huo unaotekelezwa na shirika la CRS kwa kushirikiana na Caritas pamoja na wadau wengine chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya, unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka minne katika Mkoa wa Kigoma nchini Tanzania na eno la Mpumalanga nchini Zambia ukiwa na lengo kuu ni kuhamasisha matumizi sahihi ya taka kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi sambamba na kulinda mazingira ya maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika.