Joy FM
Joy FM
13 August 2026, 14:52

Wadau wa maendeleo Manispaa ya Kigoma Ujiji wameeleza kuwa vijana hawana budi kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali zitakazowasaidia kujipatia kipato.
Na Sadik Kibwana
Vijana katikaa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkoani Kigoma, wamehimizwa kujitambua, kulinda amani ya nchi na kuwa mstari wa mbele katika shughuli za uzalishaji mali ili kujenga maisha bora na kuinua uchumi wao.
Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Kigoma Youth Development and Allied (KIVIDEA) Mkoani Kigoma.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Vijana wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw. VenanceRichard Kasimo, amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, huku wakijiepusha na makundi rika yasiyokuwa na tija katika maendeleo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KIVIDEA, Babu Pasco, amewataka vijana kuchukua hatua na kujikita katika shughuli za maendeleo zitakazowawezesha kujitegemea kiuchumi.
Amesema KIVIDEA itaendelea kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi mbalimbali, huku akiwataka kutumia maarifa wanayopata katika kujenga maisha yao.
Naye Mratibu wa Taasisi ya KIVIDEA, Zabron Joseph, amesema maadhimisho hayo yamefanikisha lengo la kuwafikishia vijana elimu na uelewa kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya maendeleo yao.
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuchagua njia sahihi za kufikia malengo yao ili kuwa na maisha bora na familia zenye msingi imara hapo baadaye.

Baadhi ya vijana walioshiriki katika maadhimisho hayo wamesema wamepata elimu, maarifa na hamasa ya kujitegemea kupitia shughuli mbalimbali zilizofanyika.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo: “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.”
Kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kushiriki katika maendeleo, bila kujali mazingira wanayoishi au changamoto zinazowakabili.