Joy FM

Madereva walia na ukosefu wa stendi Kibirizi Kigoma

20 August 2026, 11:09

Baadhi ya magari yakiwa yamebaki barabarani, Picha na Lucas Hoha

Kata ya Kibirizi ni miongoni mwa Kata zenye mwingiliano wa watu kutokana na shughuli mbalimbali za biashara zinazofanyika katika eneo hilo na kutokana na sababu hiyo vyombo vya usafiri lazima ziwepo na uhitaji wa stendi ni jambo muhimu

Na LucaS Hoha

Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto vinavyosafirisha abiria kutoka Soko la Kibirizi kwenda Ujiji na maeneo mengine ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, wameiomba Serikali kuwajengea stendi ya magari katika Kata ya Kibirizi ili kuondokana na adha ya kupaki magari pembezoni mwa barabara.

Madereva hao wamesema ukosefu wa stendi katika eneo hilo umesababisha msongamano wa magari na kuongeza hatari ya ajali kutokana na ufinyu wa eneo la maegesho.

Baadhi ya magari yakiwa yamebaki barabarani, Picha na Lucas Hoha

Wakizungumza na Radio Joy FM, baadhi ya madereva wanaopaki magari yao katika eneo la Soko la Kibirizi wamesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu, hali ambayo imekuwa kero kwao pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Wamesema magari yanapopaki kando ya barabara, eneo hilo huwa na msongamano mkubwa na hivyo kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Sauti ya madereva

Naye Diwani wa Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mrisho Mwamba, amesema suala hilo tayari ameshaliwasilisha katika kikao cha Baraza la Madiwani na kuwa kuna mpango wa kujenga stendi katika kata hiyo, huku akieleza kuwa mikakati ya awali imewekwa ili kupunguza msongamano wa magari katika Mwalo wa Kibirizi.

Sauti ya diwani wa Kibirizi

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Ramadhan Kalukula, amesema Serikali imepanga kujenga stendi hiyo ndani ya soko linaloendelea kujengwa katika eneo la Mwalo wa Kibirizi.

Amesema ujenzi wa stendi hiyo unalenga kuwaondoa madereva katika maeneo ya barabarani na hivyo kupunguza msongamano pamoja na ajali ambazo zimekuwa zikitokea katika eneo hilo.

Sauti ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Ramadhan Kalukula