Joy FM

Mwang’onda ataka wahandisi kuimarisha usimamizi wa miradi Kigoma

12 September 2026, 22:38

Muonekano wa shule ya sekondari Msimba ambayo imewekewa jiwa la msingi na mbio za mwenge wa uhuru, Picha na Lucas Hoha

Utekelezaji wa mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, ofisi, jengo la utawala, maktaba, TEHAMA, maabara na matundu 13 ya vyoo

Na Lucas Hoha

Wanafunzi katika Kijiji cha Msimba, Kata ya Mugonya, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mkoa wa Kigoma ambao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya umbali mrefu wa kwenda shule ya sekondari Luiche, sasa wameondokana na adha hiyo baada ya Serikali kujenga shule ya Sekondari Msimba kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600.

Ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwabili wanafunzi ikiwemo kuacha shule na baadhi ya wanafunzi kupata ujauzito unaohusishwa na safari ndefu ya kwenda na kurudi shuleni.

Muonekano wa shule ya sekondari Msimba, Picha na Lucas Hoha

Wanafunzi hao wakizungumza na mara baada ya Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa 2026 kuweka jiwe la msingi katika shule hiyo, baadhi ya wazazi wamesema ujenzi wa shule hiyo ni suluhisho la changamoto iliyowatesa kwa muda mrefu.

Aidha baadhi ya wazazi wa kijiji cha Kazegunga kata ya Mungonya  wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya elimu katika maeneo ya vijijini, wakieleza kuwa uwepo wa shule hiyo karibu na makazi ya wanafunzi utasaidia kupunguza changamoto za usafiri na umbali, pamoja na kuongeza fursa kwa watoto kuendelea na masomo.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba alisema ujenzi wa shule ya Sekondari Msimba ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali kuongeza nafasi za wanafunzi kupata elimu kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu kwa wakati mmoja Darasa la Sita na Darasa la Saba mwaka 2027.

Naibu waziri wa Katiba na Sheria Zainabu Katimba, Picha na Lucas Hoha

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule hiyo imekamilika, huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Chiriku Chilumba, kuhakikisha Halmashauri inatenga fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya kujenga uzio wa shule hiyo.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa shule ya sekondari Msimba, Picha na Lucas Hoha

Mwang’onda alisema ujenzi wa uzio utasaidia kuboresha usalama na mazingira ya shule hiyo ili yaendane na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya elimu.

Ujenzi wa shule ya Sekondari Msimba unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto wa eneo hilo na kupunguza changamoto zinazoweza kuwafanya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba 2026, ukilenga kukabiliana na changamoto ya mahitaji ya Madarasa, kufuatia wanafunzi wa Darasa la Sita na Saba kuhitimu pamoja Mwaka 2027 na kujiunga na Kidato cha Kwanza 2028