Joy FM

DC Kasulu kufunga soko kama usafi hautafanyika

31 August 2026, 14:01

Baadhi ya wananchi wakiwa na jeshi la polisi kufanya usafi wa mazingira, Picha na Hagai Ruyagila

Usafi wa mazingira ni jambo muhimu sana katika maisha ya kila siku ya binadamu. Mazingira safi ni yale ambayo hayana uchafu kama taka, maji machafu, vyakula vilivyooza na vitu vingine vinavyoweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu. Kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yake yanakuwa safi na salama

Na Hagai Ruyagila

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amesema atalifunga Soko Kuu la Kumsenga lililopo Mjini Kasulu mkoani Kigoma endapo wafanyabiashara na uongozi wa soko hilo watashindwa kuzingatia usafi wa mazingira.

Kanali Mwakisu ametoa kauli hiyo wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililoendeshwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma katika soko hilo, ambapo amesema hali ya usafi katika baadhi ya maeneo, ikiwemo meza za wafanyabiashara na mitaro ya kupitisha maji, hairidhishi.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila

Amesema hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za wananchi na kuongeza hatari ya mlipuko ya magonjwa, hivyo ameuagiza uongozi wa Soko la Kumsenga pamoja na wafanyabiashara kuhakikisha mazingira ya soko hilo yanakuwa safi wakati wote, vinginevyo hatua za kulifunga soko zitachukuliwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Philemon Makungu, amesema zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wananchi katika kuimarisha usalama, amani pamoja na usafi wa mazingira katika maeneo yao, huku akiwataka wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli zinazolenga kuboresha mazingira na ustawi wa jamii.

Baadhi ya wafanya biashara wa Soko hilo wamesema wamepokea maagizo hayo na watahakikisha soko hilo lina kuwa safi wakati wote ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja ili kuepuka changamoto ya magonjwa ya mlipuko ambayo ni changamoto katika afya ya mwanadamu.