Joy FM
Joy FM
13 September 2026, 11:51

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 zimewasili katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkoani Kigoma, ambapo Mwenge huo unatembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Na Lucas Hoha
Ukiwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwenge wa Uhuru umeshazindua Bweni la Wavulana katika Shule ya Sekondari Buronge, lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 156, pamoja na kukagua mradi wa vijana wa utengenezaji wa sabuni unaotekelezwa katika eneo la SIDO Kigoma, wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo ya vijana pamoja na walimu ambao wamenufaika na mradi wa ujenzi wa bweni hilo, wamesema utekelezaji wa miradi hiyo ni ishara ya namna Serikali inavyoendelea kuwajali wananchi na kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi.
Wamesema uwepo wa bweni hilo utawasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora na salama, huku mikopo kwa vijana ikiwawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Lovocatus Chipando, ameipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwawezesha vijana kiuchumi.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya kiwanda cha SIDO Kigoma ili kiwe cha kisasa na kuwawezesha wajasiriamali kufanya shughuli zao katika mazingira bora na rafiki.

Akizungumza wakati wa kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika baadhi ya miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha inaboresha maisha ya wananchi, hususan vijana.
Amesema utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vijana ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia shughuli za ujasiriamali.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 zinaendelea katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, huku Mwenge huo ukiendelea kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbio hizo zinaongozwa na kaulimbiu inayosema: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”