Joy FM

Wananchi watahadharishwa dhidi ya mvua za El Nino Kasulu

23 September 2026, 16:31

Baadhi ya wananchi, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali imeendelea kuhamasisha jamii kuhakikisha inachukua hatua dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za El nino

Na Hagai Ruyagila

Wananchi wa kata ya Msambala, Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi oktoba mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo wa kata ya Msambala, Mwesa Kaluguru, wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo.

Amesema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema, hususan wakulima, kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

Afisa Kilimo kata ya Msambala, Picha na Hagai Ruyagila

Aidha, amewasisitiza wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhama kwa wakati na kwenda maeneo salama, ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.

Kwa upande wake, Mchungaji kiongozi wa Kanisa la FPCT Hwazi, Eliya Mavyondi, amesema wapo waliokata tamaa na kuacha kulima baada ya kupata taarifa za mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni, lakini amewahimiza kuendelea kumwamini Mungu na kutokata tamaa na kuendelea kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu mpya wa kilimo.

Mchungaji kiongozi wa kanisa la FPCT Hwazi, Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya wananchi wa kata ya Msambala wamesema wameipanga na kuzingatia ushauri huo unaotolewa na wataalamu huku wakichukua hatua za mapema kukabiliana na athari za mvua hizo.

Pia wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya mvua hizo ili wananchi waendelee kuchukua tahadhari zaidi.