Joy FM
Joy FM
10 November 2026, 10:42

Katika dunia ya sasa, teknolojia imeendelea kukua kwa kasi kubwa ni kweli kwamba simu janja zina faida nyingi katika kupata elimu, mawasiliano na burudani hata hivyo, matumizi mabaya ya simu janja yanaweza kuleta madhara makubwa katika maisha ya watoto, hasa pale wanapokosa usimamizi na mwongozo kutoka kwa wazazi na walezi
Na Sofia Cosmas
Wazazi na walezi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wametakiwa kusimamia kwa karibu matumizi ya simu janja kwa watoto ili kuepusha athari zinazoweza kuathiri makuzi na maadili yao.

Wito huo umetolewa wakati wa mahafali ya watoto wa elimu ya awali katika Shule ya Platonic Day Care iliyopo Kazegunga, Wilaya ya Kigoma.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Westernbay Group Limited Kigoma, Kigunga Gerson, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanatumia simu janja kwa uangalizi na kwa kuzingatia umri wao, akieleza kuwa matumizi yasiyosimamiwa yanaweza kuwaathiri watoto katika makuzi yao.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kigoma, Exavery Nkyami, amewataka wazazi na walezi kuongeza uangalizi kwa watoto wanapotoka na wanaporejea nyumbani, ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kufanyiwa watoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Platonic Day Care, Mwalimu Elirehema Zacharia Simon, amewahakikishia wazazi kuwa shule hiyo inaweka kipaumbele katika usalama na malezi bora ya watoto.
Nao baadhi ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo wameitaka jamii kushirikiana katika kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, wakieleza kuwa watoto ni msingi wa taifa na wanahitaji kulindwa na kulelewa katika mazingira salama.

Shule ya Platonic Day Care ilianza ikiwa na watoto watano, lakini kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 110 na katika mahafali hayo, wanafunzi 41 wamehitimu elimu ya awali, huku shule hiyo ikitarajia kuanza kupokea wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka 2027.