Joy FM

DC Uvinza ataifisha boti 14 za uvuvi

23 November 2026, 09:14

Mkuu wa Wilaya Uvinza akiwa ameambatana na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama, Picha na Mwandishi wetu

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kudhibiti uharibifu wa misitu na kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika mwambao wa Ziwa Tanganyika zinafuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Mtela Mwampamba, ameamuru kutaifishwa kwa boti 14 za mizigo na uvuvi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 4.8, zilizokuwa zikitengenezwa kinyemela katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, Kijiji cha Kabeba, Kata ya Mwakizega.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo hilo, Mwampamba amesema boti hizo zenye uwezo wa kubeba tani 200 kila moja zimebainika kutengenezwa bila vibali halali, huku mbao na magogo yaliyotumika katika ujenzi wake yakidaiwa kutoka kwenye uharibifu wa mazao ya misitu yaliyohifadhiwa kisheria.

Akitoa msimamo wa Serikali kuhusu sakata hilo, Mwampamba amesema hatua hiyo inalenga kukomesha vitendo vya uvunjifu wa sheria na kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa dhidi ya matumizi yasiyo halali.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Uvinza

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ukaguzi katika eneo hilo umebaini uwepo wa gesti bubu iliyokuwa ikitumika kuhifadhi kiasi kikubwa cha mbao za miti aina ya mitipoli pamoja na mkaa.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Mtela Mwampamba, Picha na Mwandishi wetu

Kutokana na hali hiyo, ametoa maagizo ya kufungwa kwa eneo hilo mara moja na kutaifishwa kwa mazao yote ya misitu yaliyokutwa yakihifadhiwa hapo.

Mwampamba amesema uchunguzi wa kina utafanyika pia dhidi ya watumishi wa Serikali waliokuwa wakitekeleza majukumu yao katika eneo hilo, ili kubaini namna uharibifu huo ulivyoweza kuendelea licha ya uwepo wa viongozi na maafisa mbalimbali wa Serikali.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Uvinza

Amesisitiza kuwa haitakubalika kwa watumishi wenye dhamana ya kusimamia sheria kushindwa kutekeleza wajibu wao na kuruhusu uharibifu wa rasilimali za umma.

Akizungumzia madai ya baadhi ya watu kutumia majina ya viongozi wa juu wa Serikali kuhalalisha shughuli hizo, Mwampamba amesema hakuna mtu anayepaswa kujificha nyuma ya majina ya viongozi ili kukiuka sheria.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Uvinza

“Sitakubali mtu yeyote kutumia jina la viongozi wa juu wa Serikali kuhalalisha shughuli hizi. Hakuna kibali wala maelekezo kutoka juu yaliyotolewa kuruhusu uharibifu huu.” Alisema Mwampamba

Ameongeza kuwa kila mtumishi wa Serikali au mtu mwingine atakayebainika kuhusika katika vitendo hivyo atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.