Joy FM

Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa machinga

19 November 2026, 17:32

Mkuu wa Wilaya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, Picha na Lucas Hoha

Ujenzi wa ofisi ya machinga unatajwa kuwa utarahisisha utendaji kazi wa shirikisho hilo

Na Lucas Hoha

Shirikisho la machinga katika Mkoa wa Kigoma wameomba serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kufanyia shughuli zao za biashara ili waweze kuendelea kuchangia uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Wamesema hayo wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Machinga Mkoa wa Kigoma hafla ambayo imeshuhudiwa na viongozi mbalimbali na wadau wa Sekta ya biashara na kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashird Chuachua akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema machinga ni wajasiriamali muhimu katika nchi ndio maana Serikali imeamua kujenga ofisi zao nchi nzima.

Akizungumza katika Hafla hiyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara ndogondogo Mkoa wa Kigoma Mhe. Morani Mgina ameishukuru Serikali kwa namna ilivyothamini wajasiriamali kwa kuweka Ofisi itakayotumika katika kuunganisha Kundi hilo.

Baadhi ya wafanyabiashara na wamachinga, Picha na Lucas Hoha

Amesema Ofisi hiyo itafanya viongozi wa Machinga kujadili fursa, kuwakutanisha na Wadau mbalimbali pamoja na uratibu wa takwimu za Machinga.

Ujenzi wa ofisi hiyo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 29, huku Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya viwanda, biashara na uwekezaji Mkoa wa Kigoma Franco Nussu amesema machinga ni mnyororo muhimu katika biashara na kuwa kukamilika kwa Ofisi hiyo kunatoa nuru kwa machinga wa kujiendeleza na kukua katika biashara zao.

Sauti ya Mwandishi Lucas Hoha inasimulia zaidi