Joy FM
Joy FM
13 May 2026, 12:50

Baraza la watoto lina mchango mkubwa katika kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama, yenye upendo na heshima kwa haki zao
Na Mwandishi wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na World Vision, imefanya kikao cha Baraza la Watoto ngazi ya Wilaya kilichofanyika Mei 8, 2026 katika ukumbi wa Jengo la Vijana.
Katika kikao hicho, watoto walijadili madhara ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, familia na jamii kwa ujumla. Pia walipata elimu kutoka kwa wataalamu kuhusu namna ya kukabiliana na ukatili, ukatili wa mtandaoni pamoja na afya ya uzazi na mahusiano kwa vijana.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Wilaya ya Buhigwe, Gloria Alex Gabriel, aliishukuru Serikali kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kwa kuendelea kutoa elimu ya malezi, haki na ulinzi wa watoto. Pia alilipongeza World Vision kwa mchango wake katika utekelezaji wa afua mbalimbali za watoto na jamii wilayani humo.
Kwa upande wake, mgeni rasmi Amina Kaniki, Afisa Maendeleo ya Jamii, ambaye ni Mratibu wa dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kigoma aliwapongeza wajumbe wa baraza hilo na kuwahimiza kuendelea kutoa elimu kwa watoto wenzao katika ngazi za vijiji na kata, pamoja na kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya vitendo vya ukatili.

Aidha, Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata wametakiwa kuendelea kuyaimarisha na kuyahuisha mabaraza ya watoto kila mwaka ili kupata viongozi bora wa uwakilishi wa watoto katika vijiji, kata na wilaya.