Joy FM

Wananchi Kidyama Kasulu walia na uhaba wa maji safi

23 June 2026, 14:13

Mwenyekiti wa Mtaa huo, Bw. Yolam Mboneye Chijo, Picha na Sadick Kibwana

Maji ni rasilimali muhimu katika maisha ya binadamu na viumbe wengine wote duniani na hakuna kiumbe kinachoweza kuishi bila maji kwa muda mrefu

Na Sadick Kibwana

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Kidyama Kata ya Kigondo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji safi na salama ili kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.

Akizungumza na chombo hiki, mmoja wa wananchi hao amesema ukosefu wa maji umekuwa changamoto kubwa katika eneo hilo, ambapo wakati mwingine hulazimika kukaa hadi wiki nzima bila kupata huduma hiyo muhimu.

Sauti ya wananchi Kigoma
Mmoja wa wananchi hao, Picha na Sadick Kibwana

Naye Mwenyekiti wa Mtaa huo, Bw. Yolam Mboneye Chijo, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kubainisha kuwa uhaba wa maji safi umekuwa ukichangia kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko miongoni mwa wakazi wa eneo hilo mara kwa mara.

Sauti ya Mwenyekiti

Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo Mhe. Ayoub Ngaraba, amekiri uwepo wa adha hiyo na kueleza kuwa changamoto hiyo imetokana na kusitishwa kwa mkataba wa mkandarasi aliyekuwa anatekeleza mradi wa maji katika eneo hilo, baada ya kushindwa kwenda sambamba na kasi ya utekelezaji iliyotarajiwa.

Sauti ya Diwani
Diwani wa Kata hiyo Mhe. Ayoub Ngaraba, Picha Sadick Kibwana

Serikali imeeleza kuwa lengo lake na mpango kazi wake bado ni ule ule wa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao, ili kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi na kwa wakati kwa kila mwananchi.