Joy FM

RC Sirro aagiza kufunguliwa daraja mto Ruchugi Uvinza

24 April 2026, 09:53

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akiwa kwenye picha na viongozi na wananchi mara baada ya kutembelea mradi wa daraja mto Ruchugi

Ujenzi wa daraja la Mto Ruchugi Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma unatajwa kurahisisha shughuli za usafirishaji kati ya Kigoma na Tabora

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amemtaka Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya kiwango cha Lami Malagarasi, Ilunde hadi Uvinza (Km.51.1) kufungua daraja la mto Ruchugi lililopo wilayani Uvinza  ifikapo Aprili 25, 2026 ili kuruhusu barabara hiyo kupitika kwa Asilimia Mia moja.

Muonekano wa daraja la Mto Ruchugi, Picha na Ofisi mawasiliano Kigoma

Balozi Sirro ametoa maelekezo hayo, alipokagua ujenzi wa daraja hilo huku akisisitiza kutokamilika kwake kumekuwa kukiwalazimu watumiaji wa barabara hiyo kupita katika kipande cha vumbi, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu.

“Hakikisheni daraja hili linafunguliwa tarehe tuliyokubaliana ili wananchi waone uhalisia wa thamani ya matumizi ya fedha zao pamoja na kuthibitisha kuwa, serikali ipo kazini na inaendelea kutimiza wajibu wake katika kuwatumikia” amesisitiza Balozi Sirro.

Amesema kufunguliwa kwa daraja hilo, ni rasmi kutauunganisha mkoa wa Kigo na Tabora kwa njia ya lami, huku akitoa wito wa ulinzi na matumizi bora ya miundombinu hiyo.

Muonekano wa daraja la mto Ruchugi ambalo linatarajia kuanza kutumika, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinah Mathamani ametoa wito kwa watumiaji wa miundombinu hiyo kuzingatia matumizi bora na ulinzi wa alama za barabarani.

Mpaka kufikia Aprili 24, 2026, ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 98 ambapo kazi zinazoendelea kukamilishwa ni pamoja na ujenzi wa nguzo za kuonesha umbali na kingo za chuma kwa baadhi ya maeneo, usimikaji nguzo kuonesha mipaka ya barabara,  ujenzi kingo za zege pamoja na mitaro.

Muonekano wa daraja la mto Ruchugi ambalo linatarajia kuanza kutumika, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma