Joy FM
Joy FM
30 July 2026, 16:24

Serikali imeendelea kuboresha miradi ya maendeleo na kufikisha huduma bora kwa wananchi ambapo wametakiwa kuitunza ili iweze kudumu
Na Mwandishi wetu
Wananchi wa Wilaya ya Kakonko wanatarajia kupata huduma bora zaidi za afya, elimu na biashara kufuatia hatua nzuri ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani.
Hayo yamebainika leo, Julai 30, 2026, wakati Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa lengo la kuhakikisha inakamilika kwa ubora, kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Mhe. Fidel Chiza Nderego, amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi wa Kakonko.
Amesisitiza kuwa Kamati itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha kila fedha inayowekezwa inaleta matokeo yaliyokusudiwa na kwamba wananchi wanapata huduma zenye ubora unaostahili.
Katika ziara hiyo, Kamati imekagua ujenzi wa miundombinu ya usimamizi wa taka katika Zahanati ya Kinonko, hatua itakayochangia kuimarisha mazingira salama ya utoaji huduma za afya.
Pia ilitembelea ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Njoomlole na ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Ruyenzi, miradi inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Kamati pia ilikagua ukamilishaji wa nyumba ya mtumishi katika Zahanati ya Nyakayenzi, ujenzi wa choo cha matundu sita katika Shule ya Sekondari Rugenge, pamoja na ujenzi wa uzio, ‘landscaping’ na kibanda cha walinzi.

Aidha, ilitembelea ujenzi wa Soko Kuu la Kakonko, ambalo linatarajiwa kuongeza fursa za biashara, kukuza uchumi wa wananchi na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Ziara hiyo imetoa nafasi kwa wataalamu na wasimamizi wa miradi kuwasilisha taarifa za utekelezaji, hatua zilizofikiwa na mikakati ya kukamilisha miradi kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango inatarajiwa kufanya kikao cha majumuisho Julai 31, 2026, kwa ajili ya kupitia matokeo ya ukaguzi na kuweka maazimio yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.