Joy FM

Wajane watakiwa kupigania haki zao kisheria Kigoma

23 June 2026, 14:47

Baadhi ya wajane waliohudhuria siku ya wajane duniani, Picha na Sadick Kibwana

Wajane ni kundi muhimu katika jamii ambalo mara nyingi hukumbana na changamoto mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisheria baada ya kufiwa na wenza wao na ni muhimu kwa wajane kutambua na kupigania haki zao ili waweze kuishi maisha bora na kuchangia maendeleo ya familia pamoja na jamii kwa ujumla

Na Sadick Kibwana

Wajane mkoani Kigoma wametakiwa kutambua na kupigania haki zao kwa kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kutoa taarifa katika Dawati la Jinsia na kutumia fursa za umiliki wa mali zinazotolewa kwa mujibu wa sheria, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo katika maisha yao.

Rai hiyo imetolewa katika maadhimisho ya siku ya wajane duniani yaliyoandaliwa na Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Kasulu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Kigoma, Bi. Efetha Msija.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Kigoma, Bi. Efetha Msija. Picha na Sadick Kibwana

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bi. Msija amesema kuwa wajane wengi bado wako nyuma katika kudai haki zao za msingi na kutumia kikamilifu fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa na Serikali.

Sauti ya Afisa ustawi wa jamii

Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Masuala Mtambuka katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Bi. Lucy Njovu, amesema mmomonyoko wa maadili kwa watoto umeongezeka kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kusimamia malezi na kuyapa kipaumbele stahiki.

Sauti ya Mkuu wa Kitengo cha Masuala Mtambuka katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Bi. Lucy Njovu
Baadhi ya wajane waliohudhuria siku ya wajane duniani, Picha na Sadick Kibwana

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii, Novatus Peter, amewashauri wajane wanaokabiliwa na changamoto za kisheria kufika katika Dawati la Huduma za Kisheria ili kupata msaada na haki zao kwa wakati.

Sauti ya Afisa Maendeleo ya Jamii, Novatus Peter

Baadhi ya wajane waliohudhuria maadhimisho hayo wameishukuru Serikali kwa elimu waliyoipata, wakisema itawasaidia kutambua haki zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Sauti ya wajane Kasulu

Maadhimisho ya siku ya wajane duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni na mwaka huu, maadhimisho hayo kwa ngazi ya Mkoa wa Kigoma yamefanyika katika Wilaya ya Kasulu yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Wanawake wasioonekana, matatizo yasiyoonekana.”