Joy FM

RC Kigoma ahimiza weledi kwa wajumbe wa mabaraza ya ardhi na nyumba

20 April 2026, 13:16

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akiwaapisha wajumbe wa mabaraza ya ardhi na nyumba, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Wajumbe hawa wa mabaraza ya ardhi na nyumba ni sehemu ya mfumo wa haki unaolenga kutatua migogoro ya ardhi kwa haraka, kwa gharama nafuu, na kwa kuzingatia mazingira ya jamii husika.

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wajumbe wa mabaraza ya Ardhi na Nyumba ngazi za Wilaya kutekeleza majukuku yao kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, jambo litakalopunguza malalamiko ya wananchi kwa Serikali.

Balozi Sirro ametoa kauli hiyo mara baada ya kuwaapisha wajumbe wateule watatu watakaohudumu katika baraza la Ardhi na Nyumba katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Mmoja wa wajumbe wa mabaraza ya ardhi na nyumba akila kiapo, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Amesema mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya malalamiko na kesi zinazohusiana na masuala ya Ardhi, hivyo mabaraza hayo yanapaswa kubeba jukumu hilo kwa weledi mkubwa na kuhakikisha suluhu zinazopatikana zimezingatia haki itakayotokana na utoshelevu wa ushahidi.

Amesema, heshima ya mabaraza hayo inajengeka kwa kuhakikisha yanazingatia maadili na miongozo iliyowekwa ya utekelezaji majukumu yao badala ya kupendelea baadhi ya watu au makundi fulani.

Mmoja wa wajumbe wa mabaraza ya ardhi na nyumba akila kiapo, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigom

Wajumbe waliopishwa kuhudumu katika baraza hilo ni Agatha Mpumbiye, Jenitha Sunkilo pamoja na Emmanuel Bichwa na uapisho huo umefanyika leo Aprili 20, 2026, Katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akiwa katika Picha ya pamoja na wajumbe wa mabaraza ya ardhi na nyumba, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma