Joy FM
Joy FM
23 June 2026, 08:27

Mafunzo ya ajira mpya ni muhimu kwa kuwa yanawaandaa watumishi kuanza kazi kwa uelewa sahihi, nidhamu na ufanisi unaohitajika katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Na Mwandishi wetu
Watumishi wa ajira mpya katika kada ya afya wilayani Kakonko wametakiwa kufuata na kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za kazi wanapotekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Wito huo umetolewa leo, Juni 22, 2026, katika ukumbi mpya wa Halmashauri na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mustapha Mtungwe, wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa sekta ya afya.

“Mmepewa dhamana na Serikali; hakikisheni mnatimiza wajibu wenu ipasavyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi,” alisema Mtungwe.
Aidha, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Michael Magesa, aliwataka watumishi hao kuepuka vitendo vya rushwa, ikiwemo kutoa au kupokea fedha pamoja na vitendo vya ukatili au unyanyasaji wa kijinsia vinavyoweza kuathiri maadili ya utumishi wa umma.
Pia aliwasisitiza kuzingatia muda wa kazi, kuepuka kutoa taarifa za upotoshaji mahali pa kazi, na kutumia ipasavyo mfumo wa PEPMIS katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo aliishukuru Halmashauri na viongozi wake kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamekuwa na manufaa makubwa kwa watumishi wapya katika kuelewa wajibu wao na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.