Joy FM

RAS Kigoma ataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao

15 May 2026, 14:13

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akizungumza kikao cha Kamati ya Ulinzi wa Mama na mtoto ngazi ya Mkoa, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanalelewa katika mazingira bora yenye maadili mema na usalama na njia muhimu ya kutimiza jukumu hilo ni kufuatilia mienendo ya watoto wao kwani kujua mienendo ya watoto huwasaidia wazazi kuhakikisha usalama wa watoto wao.

Na Mwandishi wetu

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema wazazi wanapaswa kuongeza ufuatiliaji wa mienendo ya watoto wao hususani nyakati za likizo ili kubaini uwepo wa viashiria na vitendo vya ukatili dhidi ya kundi hilo ndani ya familia na katika jamii kwa ujumla.

Rugwa ametoa wito huo alipofungua kikao cha Kamati ya Ulinzi wa Mama na mtoto ngazi ya Mkoa, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mei 15, 2026.

Baadhi wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi wa Mama na mtoto ngazi ya Mkoa, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Amesema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikitendeka katika ngazi ya familia hususani nyakati za likizo huku wazazi na walezi wakishindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu au utaratibu wa kufuatilia changamoto hiyo.

Aidha, Rugwa amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuongeza nguvu katika kuweka mipango madhubuti itakayosaidia kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu mkakati wa Ulinzi wa mwanamke na mtoto ili kuhakikisha makundi hayo yanakua salama.

Kupitia kikao hicho, wajumbe wameitaja mikakati kadhaa yenye lengo la kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuwakumbusha watumishi wa Umma na Sekta binafsi, kutumia muda wao baada ya kazi kwa kukutanana watoto hususani nyakati za jioni na kuwasikiliza ili kubaini iwapo kuna viashiria au vitendo vya ukatili wamekua wakifanyika wawapo shuleni au wanapobaki nyumbani.

Wamebainisha kuwa, kumekuwepo na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wa shule kwenye vyombo vya usafiri wanapoelekea au kurudi shuleni au katika mazingira ya shule ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wanaohusika kuwasafirisha, walimu, wanafunzi wenzao na hata baadhi ya wanajamii wanaozunguuka maeneo ya shule.

Aidha kupitia kikao hicho, wajumbe wamesisitiza uongozi wa Kamati ngazi ya Mkoa, kuhakikisha halmashauri zinaongeza kasi katika kutekeleza Afua zinazolenga kuimarisha Ulinzi wa Mwanamke na mtoto.