Joy FM

Wanunuzi wa mazao wakutana na changamoto ya mizani Kigoma

19 May 2026, 16:01

Meneja wa Wakala wa vipimo Mkoa Kigoma, Laurent Kabikiye, Picha na Mwndishi wetu

Siku ya Vipimo duniani huadhimishwa kila tarehe 20 Mei kila mwaka na siku hii inalenga kuhamasisha matumizi sahihi ya vipimo katika biashara, viwanda na maisha ya kila siku na vipimo sahihi vina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na kulinda haki za wananchi, hasa wauzaji na wanunuzi wa mazao.

Na Mwandishi wetu

Wakala wa vipimo (WMA) mkoa Kigoma imesema kuwa wanunuzi wa mazao na madalali wa mazao wanaokwenda vijijini kununua mazao moja kwa moja kwa  wakulima wamekuwa changamoto kubwa katika suala la uzingatiaji wa vipimo na hivyo kuwanyonya wakulima.

Meneja wa Wakala wa vipimo Mkoa Kigoma, Laurent Kabikiye amesema hayo  akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma kuelekea maadhimisho ya siku ya vipimo duniani inayofanyika Mei 20 mwaka huu alisema kuwa juhudi za pamoja zinahitajika kuhakikisha wanunuzi wa mazao vijijini wanazingatia vipimo vyenye uzito unaojulikana.

Kabikiye amesema kuwa kuna wakati wanunuzi na madalali wao wananunua mahindi kwa kutumia madebe wakimaanisha debe moja ambalo linajazwa hadi juu na kuwa na ushungi wakati likipimwa kwenye mizani linakutwa na uzito wa Zaidi ya debe moja la kilo 20 hivyo kuwanyonya wakulima.

Pamoja na hilo amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya kuzingatia uzito halisi wa kisheria kwa bidhaa na huduma zote sambamba na kufanya ukaguzi na kuchukua hatua kwa wale wote wanaochezea vipimo na mizani.

Akizungumzia uzingatiaji wa vipimo kwenye bidhaa Meneja wa Mkoa Kigoma wa Chama Cha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo (NCCA), Prosper Guga amesema kuwa suala la kuzingatia vipimo ni muhimu katika suala la biashara kwani limesababisha changamoto kubwa kwa wafanyabishara wa mkoa Kigoma hasa biashara za kuvuka mpaka  ambao wamekuwa hawazingatii vipimo halisi vilivyopo kwenye nembo za bidhaa zao jambo lililofanya wengi kupoteza biashara.

Guga amesema kuwa mkoa Kigoma una fursa kubwa ya biashara na nchii za ukanda wa maziwa makuu lakini baadhi ya wafanyabiashara wamepoteza uaminifu kutokana na kile kinachokutwa kwenye bidhaa zao kuwa tofauti na maelezo yaliyopo kweye bidhaa hizo hasa katika kuzingatia uzito na ujazo wa bidhaa husika.