Joy FM

DC Kigoma apiga marufuku ufyatuaji tofali eneo la makazi

19 May 2026, 16:32

Mkuu wa Wilaya Kigoma Picha na Mwandishi Joy Fm

Hatua hiyo ni baada ya wananchi wenye makazi yao katika eneo hilo kulalamikia athari zilizoanza kujitokeza kutokana na shughuli za uchimbaji udongo kwa ajili ya tofali ambazo zimesababisha mashimo yanayotuamisha maji jirani na makazi yao na kuhatarisha usalama wa nyumba zao pamoja na athari nyingine

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, amezuia na kupiga marufuku shughuli za ufyatuaji tofali katika eneo la Kigamboni lililoko mtaa wa Butunga, Kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji, kutokana na athari za kimazingira zinazosababishwa na shughuli hizo.

Kulingana na Mwenyekiti wa Mtaa wa Butunga Hamisi Yasini, pamoja na Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Joseph Makelemo, wakati wakitoa maelezo kuhusu eneo hilo mbele ya kamati ya usalama ya wilaya, mwaka 2022 wananchi na halmashauri waliafikiana kuwa eneo hilo liwe la makazi ambapo hatua za upimaji viwanja zilifanyika.

Sauti ya Mwenyekiti na Afisa ardhi

Hata hivyo baadhi ya watu wameendelea kutumia viwanja vyao kama migodi ya ufyatuaji tofali kama shughuli ya kujiingizia kipato huku shughuli hizo zikileta athari kwa watu wengine waliojenga makazi yao katika eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi wenye makazi katika eneo hilo wameiomba serikali kuchukua hatua za kusitisha shughuli hizo, na kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa ili watoto waweze kuvuka kwenda shuleni wakati huu ambapo shule haijajengwa katika eneo hilo la makazi mapya.

Sauti ya Mkazi wa Mtaa wa Butunga

Kisha Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, aliyeongoza kamati ya usalama kwenda kujionea athari za kimazingira katika eneo hilo, akatoa maelekezo ya serikali.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma