Joy FM

Wananchi wafyatua tofali kuendeleza miradi ya maendeleo Buhigwe

14 July 2026, 15:03

Baadhi ya wananwake walioshiriki katika ufyatuaji wa matofali, Picha na Mwandishi wetu

Ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo inasaidia katika ulinzi wake na hata kusonga mbele

Na Mwandishi wetu

Zaidi ya wananchi 3,000 wa Kata ya Mwayaya, Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wamejitolea kufyatua matofali kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ilikwama kutokana na sababu mbalimbali.

Mmoja wa wananchi hao akifyatua tofauli, Picha na Mwandishi wetu

Zoezi hilo la ufyatuaji wa matofali linalenga kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo hilo, ikiwemo miradi ya elimu, afya na miundombinu mingine ya kijamii, kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Wananchi hao wamesema ushiriki wao katika shughuli hizo ni sehemu ya mchango wao katika kuharakisha maendeleo ya kata hiyo na kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakamilika kwa wakati.

Diwani wa Kata ya Mwayaya, Ephraim Raymond Sibanganya, amesema wananchi wa kata hiyo wanatarajia kufyatua zaidi ya matofali laki 1 yatakayotumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii kwa wakazi wa eneo hilo.

Askari Polisi akishirikiana na wananchi waliojitolea kufyatua tofali, Picha na Mwandishi wetu

Aidhaa ameongeza kuwa mwitikio mkubwa wa wananchi katika zoezi hilo unaonesha dhamira yao ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu mbalimbali.