Joy FM

NMB yakabidhi madawati 150 Kakonko

24 June 2026, 17:51

Ni muonekano makabidhiano ya madawati mbele ya wananfunzi, Picha na mwandishi wetu

Walimu walipokea madawati hayo wametakiwa kutatunza ili yaweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu

Na Mwandishi wetu

Benki ya NMB imekabidhi madawati 150 kwa shule mbalimbali za Wilaya ya Kakonko katika hafla iliyofanyika leo, Juni 24, katika Shule ya Msingi Kiyobela.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mustapha Mtungwe, Afisa Elimu ya Awali na Msingi, Isabella Mwakabonga, Mdhibiti Ubora wa Shule Wilaya, Japhet Mbaga pamoja na Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Kakonko Bi.Elizabeth Kanjagaile.

Wanafunzi wakiwa wamekalia madawati yalitolewa na NMB, Picha na Mwandishi wetu

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Elimu ya Awali na Msingi, Isabella Mwakabonga ameishukuru Benki ya NMB kwa mchango huo mkubwa ambao unaenda kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa wilaya hiyo.

Amesema madawati hayo yatasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa samani za shule na kuongeza ari ya wanafunzi katika masomo.

Baadhi ya viongozi na walimu pamoja na wanafunzi wakifurahia baada ya mapokezi ya madawati, Picha na Mwandishi wetu

Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kakonko, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kusaidia sekta ya elimu kadri itakavyowezekana.

Naye Mdhibiti Ubora wa Elimu Wilaya ameishukuru NMB kwa moyo wake wa kujitolea na kuahidi kufuatilia matumizi sahihi ya madawati hayo ili yafikie lengo lililokusudiwa.

Akihitimisha hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Mustapha Mtungwe aliwataka walimu, wanafunzi na kamati za shule kuyatunza madawati hayo kwa umakini ili yadumu kwa muda mrefu na kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Amesisitiza kuwa utunzaji bora wa miundombinu ya elimu ni msingi muhimu wa kuinua ufaulu na maendeleo ya wanafunzi.