Joy FM
Joy FM
20 May 2026, 14:22

Maendeleo ya wananchi ni jambo muhimu katika taifa lolote duniani na ili wananchi waishi maisha bora, ni lazima kuwepo ushirikiano kati ya serikali na taasisi za dini. katika kuhakikisha jamii inapata huduma muhimu kama elimu, afya, usalama, na maadili mema
Na Hagai Ruyagila
Serikali Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma imesema itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kudumisha amani katika wilaya hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele, wakati akizungumza na wachungaji pamoja na wenzi wao katika kanisa la Mt. Andrea Anglikana Kasulu Mjini.
Bi, Mtewele amesema taasisi za kidini zina mchango mkubwa hususan katika kudumisha amani, maadili na kuhamasisha maendeleo kwa wananchi jambo ambalo limekuwa likiunga mkono jitihada za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Askofu wa Dayosisi ya Western Tanganyika Kanisa Anglikana Tanzania, Mhashamu Emmanuel Bwatta, amesema serikali imeendelea kufanya maendeleo makubwa wilayani humo hususan katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya barabara.

Hata hivyo, Askofu Bwatta ameiomba serikali kuwatumia wakazi wa Kasulu na mkoa wa Kigoma katika miradi mbalimbali inayofanyika wilayani humo ukiwemo wa SGR ili waweze kupata ajira na kujiongezea kipato, badala ya kuwatumia watu kutoka nje ya mkoa wakati baadhi ya kazi hizo zinaweza kufanywa na wananchi wa Kigoma.
Mchungaji Bhikolimana Abrahamu bhitona amesema ni muhimu kwa serikali kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuboresha miundombinu ya barabara na huduma nyingine ili kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, wananchi na taasisi za dini.