Joy FM

ENABEL yatoa mafunzo kwa wanawake viongozi Kasulu

2 June 2026, 12:32

Washiriki wa mafunzo ya viongozi wakiwa katika semina, Picha na Mwandishi wetu

Wanawake ni sehemu muhimu ya jamii na wana mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa na ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ni muhimu wapatiwe elimu na mafunzo ya uongozi

Na Mwandishi wetu

Shirika la Enabel limeendelea kutoa fursa mbalimbali katika jamii ambapo wanawake viongozi wapatao 20 kwa ngazi ya umma mkoani kigoma wamepatiwa mafunzo ambayo yatawasaidia katika kufanya shughuli zao kwa kujiamini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika wilayani Kasulu, Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani amesema ni muhimu wanawake kujitambua na kuimarisha uwezo katika nyanja tofauti  hasa katika mitandao ya kitaaluma.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani
Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani, Picha na Mwandishi wetu

Awali akitoa taarifa ya mradi huo wa wezesha binti Jovitha Mlay mtaalamu wa maswala ya jinsia kutoka Enabel amesema mafunzo hayo yatadumu kwa muda wa miezi 8 na wanawake 20 kutoka wilaya zote za mkoa watashiriki mafunzo ili waweze kuwa chachu ya kuwasaidia wanawake wenzao

Mlay ameongeza kuwa hii ni sehemu ya kuleta mabadiliko  katika taasisi za umma na watakuwa mfano wa kuigwa kwa wasichana wanaohudumiwa na mradi wa wezesha biti hivyo kasi ya mabadiliko katika uongozi itakuwa kubwa.

Sauti ya Jovitha Mlay

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu mji Mwl. Vumilia Simbeye amewapongeza Enabel kwa kuwawezesha wanawake viongozi kupata mafunzo hayo kwani ni fursa ya kuwatoa hatua moja kwenda nyingine.

Sauti ya Vumilia Simbeye

Baadhi ya washiriki akiwemo Atuketile Mwasalemba na Renata Magayane wamesema mafunzo watakayopata yatakwenda kubadili mtazamo hasi kati jamii kwamba mwanamke hawawezi uongozi bali ni kuwajengea uwezo wa kuthubutu na kutenda bila kujali tofauti ya kijinsia.

Sauti ya Wanufaika