Joy FM
Joy FM
24 June 2026, 09:48

Mradi huu utaimarisha huduma za usafiri wa anga kwa kuongeza uwezo wa kiwanja kuhudumia ndege kubwa zaidi na itarahisisha usafiri wa abiria na mizigo kutoka Kigoma kwenda maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi
Na Mwandishi wetu
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imesema kuwa mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha NdegeKigoma umefikia asilimia 60 ya utekelezaji.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elisony Mweladzi, amesema uboreshaji wa kiwanja hicho ulianza Septemba 2023 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 34, huku ukitarajiwa kukamilika Julai 2026.

Mhandisi Mweladzi amesema mradi huo unatekelezwa na China Railway Construction Engineering Group kwa gharama ya shilingi bilioni 51.4.
Hadi sasa, mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 24.5 kwa kazi zilizotekelezwa. Ameeleza kuwa kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa maegesho ya ndege yenye uwezo wa kuhudumia ndege kubwa tisa aina ya Boeing
737 – 800 kwa wakati mmoja, tofauti na awali ambapo kiwanja hicho kilikuwa na uwezo wa kuhudumia ndege ndogo aina ya Bombardier Q400 pekee.
Kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (runway) yenye urefu wa kilomita 1.8, barabara za ndani zenye urefu wa kilomita 1.5, pamoja na maegesho ya magari yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya magari 100 kwa wakati mmoja.

Aidha, Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500 kwa wakati mmoja,jengo la kuongozea ndege na jengo la vifaa vya umeme vya taa za kuongozea ndege.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mweladzi, mradi huo ukikamilika utakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuimarisha usafiri wa anga katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mradi huo pia unatarajiwa kuongeza fursa za biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine nchini.
Akimshukuru Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhandisi Mweladzi amesema upatikanaji wa fedha za mradi umewezesha utekelezaji wake kuendelea bila changamoto za malipo kwa Mkandarasi.