Joy FM
Joy FM
8 May 2026, 14:31

Halmashauri ya Mji wa Kasulu mKoani Kigoma imeendelea kufanya vizuri katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini uongozi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mwl. Vumilia Simbeye
Na Mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye kwa namna anavyoendelea kuwahudumia wananchi na kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo.
Chidebwe amebainisha hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika mjini Kasulu, ambapo amesema uongozi wa halmashauri umeonyesha ushirikiano mzuri kwa wananchi katika kutoa huduma pamoja na juhudi za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Amesema huduma zinazotolewa chini ya usimamizi wa mkurugenzi huyo zimeendelea kuimarika na kusaidia kuongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, amesema ushirikiano kati ya viongozi, watumishi wa umma na wananchi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya wilaya hiyo.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtelewe, amewasisitiza madiwani kuendelea kujenga mahusiano mazuri kati ya serikali na wananchi namna ambavyo serikali imefanya ili kusaidia kuimarisha maendeleo pamoja na kudumisha mshikamano katika jamii.
Amesema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi serikalini.
