Joy FM
Joy FM
23 July 2026, 08:54

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Sirro ameutaka uongozi katika Halmashauri za Mkoa kutosita kuwachukulia hatua watendaji wanaosababisha hoja sambamba na wakusanya mapato wasio waadilifu wanaosababisha upotevu wa fedha za makusanyo.
Na Mwandishi wetu
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Halmashauri za Wilaya Buhigwe, Kasulu na Mji Kasulu zimefanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha 2024/2025.
Akitoa taarifa kupitia Mikutano ya mabaraza Maalum ya Madiwani ya kujadili Hoja na za Ukaguzi yaliyofanyika Julai 22, 2026 katika Halmashauri hizo, Mkaguzi Mkuu wa nje wa Mkoa wa Kigoma, CPA. Honest Muya amesema uwajibikaji ndio msingi Mkuu wa kuondokana na hoja za Ukaguzi katika Halmashauri.
Amesema baadhi ya hoja hujitokeza kutokana na ukosefu wa nyaraka au kutowasilisha kwa nyaraka hizo kwa wakati, jambo ambalo wataalam wanaweza kukaa pamoja na kulishughulukia na hoja zikajifuta.
Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amezipongeza Halmashauri hizo huku akisisitiza kufanyiwa kazi kwa hoja chache zilizopo ambazo nazo pia zinaweza kupata utatuzi.

Aidha kupitia Mabaraza hayo, Balozi Sirro amehimiza matumizi ya daftari kwa ajili ya kutambua wakazi kwenye ngazi za vitongoji, vijiji na Mitaa ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Madiwani kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa miradi katika maeneo Yao badala ya kusubiri mpaka wananchi waanze kulalamika.