Joy FM

Vikundi 53 vyapatiwa mikopo ya shiligi milioni 608.9 Kasulu

29 June 2026, 08:36

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akikabidhi hundi ya mikopo kwa wawakilishi wa vikundi, Picha na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 608,965,100 kwa vikundi 53 vya wajasiriamali kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo ya robo ya tatu na ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amesema mikopo hiyo inalenga kuongeza uwezo wa wanufaika kujiongezea kipato, kupanua shughuli za kiuchumi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo kwa vikundi Kasulu, Picha na mwandishi wetu

Mikopo ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi kwa kuwa huwapa wananchi fursa ya kuanzisha au kupanua shughuli za uzalishaji na biashara

Na Mwandishi wetu

Rugwa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha, akieleza kuwa fedha hizo zimekuwa zikielekezwa kwenye shughuli zilizokusudiwa, jambo linaloonyesha uwajibikaji na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mhe. Charles Kadogo, amewataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaack Mwakisu, amesema ameridhishwa na ushirikiano uliopo kati ya ofisi yake na halmashauri katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali, hususan usimamizi wa mpango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani, ambao umeendelea kutekelezwa kwa ufanisi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, amesema ukusanyaji wa mapato ya ndani unaendelea kuimarika kupitia vyanzo mbalimbali vya kodi, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwani fedha hizo hurejeshwa kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akiwa kwenye picha na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya Wilaya Kasulu, Picha na Mwandishi wetu

Kwa niaba ya wanufaika, Mwenyekiti wa Kikundi cha Tushikamane Mgombe, Anatolia Tinya, amesema kikundi chao kilinufaika na mkopo wa awali, kiliurejesha kwa wakati na baadaye kikapata mkopo mkubwa zaidi uliowawezesha kupanua biashara, kujenga nyumba na kusomesha watoto hadi elimu ya juu.

Katika mgawanyo wa mikopo hiyo, vikundi vya wanawake vilipokea shilingi 281,250,000, vikundi vya vijana shilingi 300,897,600, huku vikundi vya watu wenye ulemavu vikikabidhiwa shilingi 26,817,500, na kufanya jumla ya shilingi 608,965,100 zilizotolewa kwa vikundi 53.