Joy FM
Joy FM
11 May 2026, 08:45

Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi ameeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Malagarasi Wilaya ya Uvinza unaotekelezwa na kampuni ya DONGFANG Electric International Corporationo (DEC).
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi, ameliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme nchini TANESCO kumuondoa mhandisi mkazi wa mkandarasi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Malagarasi wilayani Uvinza mkoani Kigoma, kutokana na mwenendo usioridhisha wa utekelezaji wa mradi huo.
Waziri Ndejembi, ametoa maagizo hayo baada ya kukagua mradi huo wa kuzalisha megawati 49.5 za umeme na kubaini kuwa mradi huo uko nyuma ya muda licha ya mkandarasi kulipwa fedha za awali kiasi cha Dola Milioni 20 za marekani, na pia mkandarasi amekuwa akifanya kazi kwa kufuata mawazo yake binafsi tofauti na mkataba alioufunga na TANESCO.

Amesema fedha iliyolipwa haiendani na kazi iliyofanyika hivyo pamoja na kuagiza kuondolewa kwa mhandisi mkazi wa mkandarasi wa mradi huo Duan Longhai wa kampuni ya kichina ya DONFANG ELECTRIC INTERNATIONAL CORPORATION (DEC), Waziri Ndejembi ameagiza pia ufanyike ukaguzi kwa lengo la kubaini namna fedha zilivyotumika.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro katika ziara hiyo, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuiondoa Kigoma na Taifa kwa ujumla katika changamoto ya umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange, amesema mradi wa kuzalisha umeme wa Malagarasi, unaogharimu fedha kiasi cha Milioni 144.14 Dola za kimarekani sawa na takribani Shilingi Bilioni 370 za kitanzania uko nyuma ya muda kwa zaidi ya asilimia 20%.