Joy FM
Joy FM
15 April 2026, 2:47 pm

Umuhimu wa kimataifa wa watoto wanaoishi mtaani ni suala kubwa la kijamii na haki za binadamu duniani na hii inahusisha juhudi za kulinda, kusaidia, na kuhakikisha watoto hawa wanapata haki zao za msingi
Na Mwandishi wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imeungana na wadau mbalimbali kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani, ambapo wito umetolewa kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuimarisha malezi na ulinzi wa watoto ili kupunguza na hatimaye kutokomeza tatizo la watoto wanaoishi mitaani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Franley Lucas Lazaro amesisitiza kuwa familia ndiyo msingi mkuu wa malezi ya mtoto, hivyo wazazi wanapaswa kuhakikisha wanawapatia watoto wao upendo, uangalizi, maadili mema pamoja na mwongozo sahihi wa maisha.
Amebainisha kuwa malezi bora na mawasiliano ya karibu kati ya wazazi na watoto huchangia kuwajenga watoto wenye nidhamu, kujitambua na kuepuka kujiingiza katika mazingira hatarishi ya maisha ya mitaani.

Aidha, wazazi wamehimizwa kuwajibika kikamilifu katika kuwapatia watoto mahitaji yao muhimu ikiwemo elimu, malezi bora na ulinzi, huku wakitakiwa kuwa karibu nao ili kufahamu changamoto wanazokutana nazo katika hatua mbalimbali za ukuaji wao.
Kwa upande wao, watoto waliokuwepo katika maadhimisho hayo walikumbushwa umuhimu wa kuwaheshimu wazazi na walezi wao pamoja na kuzingatia maelekezo wanayopewa, kwani nidhamu na ushirikiano huimarisha mahusiano ndani ya familia na kuwa msingi wa maisha yao ya baadaye.
Katika kuadhimisha siku hiyo, shughuli mbalimbali za michezo zilifanyika zikiwemo mpira wa miguu, mbio za magunia na kuvuta kamba ambapo washindi walipatiwa zawadi zilizotolewa na mgeni rasmi ambaye alikuwa mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo.
Maadhimisho hayo yamekuwa chachu ya kuhamasisha jamii kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye upendo na yanayowawezesha kufikia ndoto zao.