Joy FM
Joy FM
14 August 2026, 10:52

Uchumi rejeshi kutoka kwenye taka ni mfumo wa kuzifanya taka ambazo zingeonekana hazina matumizi kuwa rasilimali yenye thamani ya kiuchumi kupitia ukusanyaji, uchakataji, urejelezaji na matumizi mapya
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, amewahimiza wananchi wa Kata ya Kazuramimba na kata nyingine zinazotekeleza Mradi wa VOICES katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kuchangamkia fursa ya kiuchumi inayotokana na taka kwa kuzitenganisha, kuzichakata na kuzipa thamani.

Mh. Dinah ametoa rai hiyo leo katika Viwanja vya Soko la Kazuramimba wakati akizindua kampeni ya “TAKA NI PESA”, inayotekelezwa na Shirika la CRS kwa usaidizi wa Kampuni ya JIDI inayotoa utaalamu wa kitaalamu.
Amesema kampeni hiyo, pamoja na kusaidia kuweka mazingira safi kwa kukusanya taka katika maeneo ya biashara, makazi na mikusanyiko ya watu, itawawezesha wananchi kujipatia kipato kupitia uchumi rejeshi kwa kuzitenganisha na kuzichakata taka.

“Wananchi tusione taka kama uchafu usio na thamani, bali tuzichukulie kama fursa ya kiuchumi. Tukizitenganisha, kuzichakata na kuzipa thamani, tunaweza kujiongezea kipato huku tukilinda mazingira,” amesema Mh. Dinah.
Kwa upande wake, Afisa Afya na Mazingira wa Wilaya ya Uvinza, Bw. Hussein Kateranya, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, amewahakikishia wananchi wa Kazuramimba kuwa Halmashauri iko tayari kutoa msaada wa kitaalamu katika kuanzisha na kuendesha vikundi vya uchakataji wa taka.

Amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujipatia kipato kutokana na taka zinazozalishwa katika maeneo yao.
Naye Mratibu wa Kampeni ya “TAKA NI PESA”, Ndg. Kwaresima Kihumbi, amesema uzalishaji wa taka katika Kazuramimba na Wilaya ya Uvinza kwa ujumla ni fursa ya kiuchumi inayopaswa kupewa kipaumbele, akiwahimiza wananchi kubadili mtazamo na kuanza kuziona taka kama rasilimali yenye thamani.

Mradi wa VOICES unatekelezwa Tanzania na Zambia kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wilayani Uvinza, mradi huo unatekelezwa katika Kata za Uvinza, Nguruka, Mganza, Basanza, Ilagala, Igalula na Kazuramimba.
“TAKA NI PESA — Tenganisha leo, tengeneza mkwanja leo!