Joy FM
Joy FM
6 July 2026, 08:40

Ebola ni ugonjwa hatari wa kuambukiza unaoweza kusababisha madhara makubwa kwa afya na maisha ya watu ikiwa hautadhibitiwa mapema, kuimarisha utayari wa kukabiliana na Ebola katika Mkoa wa Kigoma ni hatua muhimu ya kulinda wananchi na kuhakikisha jamii inaendelea kuwa salama
Na Mwandishi wetu
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendesha zoezi la kupima utayari wa watalaam wa Afya na Sekta mtambuka katika kukabiliana na dharura za Afya ya Jamii ikiwemo ugonjwa wa Ebola katika Mkoa wa Kigoma.
Zoezi hilo limefanyika Julai 2 hadi 3, 2026, kwa lengo la kupima na kutathimini utendaji wa Sekta zinazohusika moja kwa moja katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kukagua mifumo ya mawasiliano na uratibu wa huduma pindi dharura inapotokea.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Zabibu Mkamba, amesema Wilaya Sita za Mkoa wa Kigoma zinapakana na nchi jirani hivyo wataalam hao wanajukumu kubwa la kuhakikisha maeneo yao yanakua salama ili kudhibiti uwezekano wa maradhi kuingia nchini na hata yakiingia basi yaweze kudhibitiwa katika hatua za awali.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Bi. Mwanaisha Mrisho, amesema zoezi hilo linatoa taswira na kuona ni kwa kiasi gani Mkoa wa Kigoma upo tayari kukabiliana na dharura za kiafya ikiwemo ugonjwa wa Ebola
Amesema kwa kiasi kikubwa watendaji hao wapo tayari kukabiliana na changamoto ya uwezekano wa kuenea kwa maradhi hayo huku akisisitiza kuwa ufanisi huo umefikiwa kutokana na serikali ya awamu ya Sita kuweka Sera Bora za kiafya na kuzisimamia kwa vitendo.

Upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Ibrahima Saleh amesema Mkoa umejiweka tayari na vituo vyote vya kufuatilia ugonjwa huo vinaendelea na majukumu.
Amesema tayari wataalam walishapata mafunzo ambapo katika hatua ya sasa zoezi la kupima utayari limezigusa Halmashauri za Wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Ameendelea kusisitiza kuwa, wameona unuhimu na matokeo ya zoezi hilo kwani limewasaidia kubaini maeneo ambayo ni mapungufu na wanatakiwa kuyafanyia kazi ili kuzidi kuimarisha utayari.