Joy FM

DED Uvinza apongeza serikali ujenzi shule ya wasichana Kigoma

20 April 2026, 08:23

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Kigoma wakiwa katika mahafali, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Watoto wa kike wanapo pata elimu wanakuwa na nafasi kubwa ya kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii na wataalamu wa elimu wanasema kuwa elimu kwa wasichana ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu katika jamii nyingi duniani.

Na Mwandishi wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza CPA Fred Milanzi ameishukuru serikali kwa kutoa fedha na kuhakikisha shule ya Wasichana ya Kigoma inajengwa wilayani Uvinza ukiwa ni mwendelezo wa jitihada za kuinua kiwango cha elimu hasa kwa watoto wa kike.

CPA Milanzi amesema hayo katika Mahafali ya kwanza na ya kihistoria katika shule ya Wasichana ya Kigoma iliyopo wilayani Uvinza.

CPA Milanzi, amewashukuru walimu kwa malezi ya wanafunzi hao, akieleza kuwa wamelelewa katika maadili makubwa na nidhamu jambo linalowaongezea kujiamini akitolewa mfano nmna walivyokuwa wakiwasilisha maonesho mbalimbali kuhusu masomo yaliyofundishwa darasani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza CPA Fred Milanzi, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Aidha amewatakia kheri katika mitihani akiamini watakwenda kufanya vizuri kwa kuipeperusja vyema shule hiyo kitaifa kwa matokeo mazuri ya kishindo.

Naye Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Uvinza Mwl Julius Kakyama amesema wakati shule inaanzishwa miundombinu mbalimbali ilikuwa haijakamilika, akifafanua kuwa mabweni yalikuwa nane na hayakuwa yamekamilika, baadhi ya madarasa na ukumbi uliotumika kuhodhi Mafahali hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa shule Mwl. Sofia Nambua Theobald ameeleza kuwa shule hiyo inajivunia kuwalea vijana hao huku akiitaja miundombinu ya shule kuwa chachu ya kusoma kwa bidii na wazazi kuhamasika kuwaleta watoto wao wa kike kwa wingi hatua inayochangia kuongezeka kwa idadi ya wasichana katika tahasusi za sayansi.

Afisa elimu na Mkuu wa shule ya wasichana Kigoma iliyopo Wilyani Uvinza, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Awali akiwasilisha risala ya kidato cha Sita mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mwanafunzi wa tahasusi ya PGM, Valeria Augustine Masele,

Kwa niaba ya wenzake ameahidi ufaulu wa daraja la juu na pia kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo hata baada ya kuhitimu masomo yao.

Wahitimu wa kidato cha sita wakiwa kwenye mahafali, Picha na Ofisi ya mawasiliano uvinza

Jumla ya Wanafunzi 139 katika tahasusi za sayansi za PGM, PCM, PCB watakuwa wanaanza mitihani ya kuhitimu kidato cha sita mapema mwezi ujao.