Joy FM
Joy FM
22 April 2026, 08:35

Madiwani ni kiungo muhimu kati ya wananchi na serikali katika kudhibiti wahamiaji haramu, hasa kwa upande wa taarifa, uhamasishaji, na ushirikiano wa kijamii.
Na Hagai Ruyagila
Mkuu wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Isaac Mwakisu amewataka Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, kushirikiana na serikali katika kudhibiti wahamiaji haramu kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuwafichua wanaoishi kinyume na sheria ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Kanali Mwakisu ametoa wito huo wakati akiwasilisha salamu za serikali katika kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kagoma.

Amesema kupitia operesheni iliyofanyika kwa kipindi cha wiki moja, wamefanikiwa kuwakamata na kuwarejesha katika nchi zao wahamiaji haramu waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria.
Aidha amewasisitiza viongozi wa kata wanapaswa kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika ili kuhakikisha udhibiti wa wahamiaji haramu unaimarika na hali ya ulinzi inaendelea kuwa tulivu katika maeneo yao.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mh. Charles Benjamini ambaye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, amesema baadhi ya viongozi wakiwemo madiwani wamekuwa wakiwakingia kifua wahamiaji haramu kutokana na kuishi nao kwa muda mrefu katika maeneo yao, hata hivyo amesema baada ya maelekezo hayo, wamekubaliana kushirikiana ili kutokomeza tatizo hilo.

Baadhi ya Madiwani wa halmashauri hiyo wameunga mkono kauli ya mkuu wa wilaya kwa kusema kuwa wahamiaji haramu wamekuwa chanzo cha uharifu ambapo wamesema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuimarisha hali ya usalama katika halmashauri hiyo.