Joy FM
Joy FM
3 July 2026, 12:56

Rushwa ni moja ya changamoto kubwa zinazokwamisha maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla kwani huathiri utoaji wa huduma za umma, hupunguza uwajibikaji na kudhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za serikali
Na Sadick Kibwana
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya hiyo kuongeza elimu ya uelewa wa rushwa kwenye maeneo yao, ili kila mwananchi afahamu madhara yake.
Tuungane na Mwanahabari Wetu Sadick Kibwana kwa Taarifa zaidi…
Wakizungumza na kituo hiki, wakazi hao wamesema wamekuwa wakiona viashiria mbalimbali vya rushwa katika utendaji wa shughuli za kila siku, lakini hawajui ni viashiria hivyo na wapi pa kutoa taarifa.

Aidha, Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Elimiliki Kihundrwa amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa serikali za mitaa, vikundi vya wanawake na vijana, ili ufahamu upatikane kwa kiwango cha chini kabisa.
Pia Mkuu huyo wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa mara moja wanapoona viashiria vya rushwa.
Aidha, TAKUKURU inaendelea na kampeni ya kitaifa ya kutokomeza rushwa inayosema “Jukumu la kutokomeza rushwa ni lako na langu. Kwa pamoja tupigane nalo”, ambayo ni mahususi kwa kila mwananchi kuipinga rushwa katika ngazi zote.