Joy FM
Joy FM
25 May 2026, 09:49

Ugonjwa wa Ebola ni hatari kubwa kwa sababu husababishwa na virusi vinavyoenea kwa haraka kupitia kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa kama damu, mate, jasho, mkojo au matapishi
Na Hagai Ruyagila
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amewataka wananchi Wilayani humo kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Ebola ambao tayari umeingia katika nchi jirani.
Kanali Mwakisu amesema hayo katika ibada ya maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Kigoma ambapo kimkoa imefanyika katika viwanja vya Kanisa la Anglikana Murusi, Mjini Kasulu.

Amesema ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari mapema ili kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Akisoma barua ya serikali kwa waumini wa dini ya Kikristo katika ibada hiyo, Mkaguzi wa Polisi na Polisi Kata wa Kata ya Nyansha, Mbaraka Luwongo, amezitaja miongoni mwa dalili zinazosababishwa na virusi vya ugonjwa wa ebola na kueleza kuwa serikali inaendelea kuchukua tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo CCT Mkoa wa Kigoma, Ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Magharibi Mhashamu Jackson Mushendwa, amewaomba waumini kuendelea kuombeana na kuwa wa moja ili kuepuka ugonjwa huo.

Baadhi ya waumini wa dini ya Kikristo wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wamesema wataendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kujilinda na kuhakikisha wanakuwa salama huku wakiiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo.
