Joy FM
Joy FM
5 June 2026, 09:40

Usimamizi wa miradi ya maendeleo una umuhimu mkubwa kwa sababu husaidia kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa ufanisi na kwa wakati
Na Mwandishi wetu
Wasimamizi wa miradi katika maeneo mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fedha za miradi kwa uadilifu kwa kutunza kumbukumbu ya manunuzi ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Wakili Emmanuel Ladislaus, wakati Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.
Wakili Ladislaus amesema usimamizi makini wa miradi ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba wananchi wanapata huduma na manufaa yanayotarajiwa kutokana na uwekezaji huo.
Katika ziara hiyo, timu ya menejimenti ilitembelea miradi inayotekelezwa katika vijiji vya Kitema, Migunga, Kurunyemi, Kurugongo, Shunguliba, Rungwe Mpya, Asante Nyerere, Kalela, Mlole na Rusesa, kwa lengo la kufuatilia maendeleo na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
Katika hatua nyingine, Timu ya Menejimenti ya Halmashauri imewapongeza wasimamizi wa miradi kwa hatua nzuri ya utekelezaji iliyofikiwa hadi sasa, huku ikiwataka kuongeza kasi ya utekelezaji ili miradi yote ikamilike kabla ya kuhitimishwa kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.