Joy FM

Rais wa Burundi aomba Rwanda kusema ukweli

1 January 2026, 14:37

Pichani Rais wa Burundi Evariste Ndayishiniye na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Picha na Bukuru Elias

Rais Evariste Ndayishimiye ameishutumu Rwanda kwa madai ya kuyumbisha usalama ukanda wa maziwa makuu na Afrika masshariki na kuwa na nia mbaya kwa nchi ya Burundi.

Katika hotuba ya mwaka mpya kwa warundi, rais Ndayishimiye alihusisha machafuko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na njama ya kuiyumbisha Burundi.

Pia aliishutumu Rwanda kwa kuwahifadhi wale wanaotaka kuyumbisha usalama wa Burundi.

Rwanda na Burundi zimekuwa na historia ndefu ya uhasama tangu Burundi ilipoingia katika mzozo wa kisiasa mwaka 2015 kutokana na uamuzi wa hayati Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu, jambo ambalo wapinzani wanasema lilikuwa kinyume cha katiba.

Mzozo huo ulichochewa na jaribio la mapinduzi Mei 13, 2015, lililoongozwa na Jenerali Godefroind Niyombare.

Burundi imeendelea kuishutumu Rwanda kwa kuwahifadhi wale waliojaribu kupindua serikali.

Katika hotuba yake, Rais Ndayishimiye alipongeza kuwa uhusiano wa nchi yake na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mzuri, isipokuwa Rwanda.