Joy FM
Joy FM
16 April 2026, 3:28 pm

Majiko banifu ni suluhisho muhimu kwa maendeleo endelevu yanayochangia afya, uchumi, na utunzaji wa mazingira
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, ametoa wito kwa wananchi wilayani humo kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda na kuhifadhi mazingira.
Dkt. Chuachua ametoa wito huo wakati wa akizindua ugawaji wa majiko sanifu ya kupikia ya gharama nafuu yenye ruzuku ya serikali, kwa wananchi katika kata ya Simbo wilayani Kigoma, ambapo amesema kuwa matumizi ya majiko sanifu ni hatua muhimu ya kubana matumizi na zaidi kulinda na kuhifadhi mazingira, kwa kuwa majiko hayo yanatumia nishati kidogo.
Kampuni ya ENVOTEC iliyopewa dhamana ya kuuza majiko hayo kwa bei ya ruzuku kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA, kwa ujumla imegawa majiko 1,404 kwa wilaya ya Kigoma, ambapo mwakilishi wa kampuni hiyo Florence Masunga, amesema wananchi watachangia asilimia 15% tu ya bei huku serikali ikilipia asilimia 85%.
Baadhi ya wananchi waliopata majiko hayo wameeleza furaha yao na namna watakavyoyatumia katika vijiji vyao.
Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndiye kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia humu nchini na Afrika, kwa lengo la kulinda na kuhifadhi mazingira, pamoja na kuwaepusha binadamu na madhara yatokanayo na matumizi ya kuni na mkaa.