Joy FM

Serikali yapokea mtambo wa kuchakata mazao ya uvuvi Kigoma

15 April 2026, 9:37 am

Miongoni mwa mitambo ilyotolewa na Serikali kwa ajili uchakaji wa mazao ya uvivu, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Mitambo ya kuchakata husaidia kubadilisha samaki na mazao mengine ya uvuvi kuwa bidhaa zenye thamani zaidi kama samaki waliokaushwa, waliogandishwa au waliowekwa kwenye makopo

Na Mwandishi wetu

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepokea mtambo wa kisasa wa kuzalisha barafu na kukaushia dagaa, pamoja na majokofu yanayotumia nishati ya jua, kutoka mradi wa FISH4ACP ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi mkoani Kigoma.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mtambo huo iliyofanyika Aprili 14, 2026 katika mwalo wa Katonga mkoani Kigoma, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhe. Hassan Rungwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema kuwa mtambo huo utawasaidia wavuvi kuongeza ufanisi katika shughuli zao na kukuza uzalishaji utakao wawezesha kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Hatua hii itaongeza ubora wa mazao ya uvuvi, kuimarisha ushindani wa bidhaa zetu katika masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuinua kipato cha wananchi wa Mkoa wa Kigoma,” amesema Mhe. Rungwa.

Katibu Tawala wa Mkoa w Kigoma Mhe. Hassan Rungwa aliyesimama, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Aidha, Mhe. Rungwa amewataka wavuvi pamoja na mamlaka zinazosimamia mradi huo kuhakikisha wanatunza mtambo huo na vifaa vyake ili uweze kudumu na kuwanufaisha wananchi pamoja na Serikali kwa ujumla.

Rungwa amefafanua kuwa, vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mtambo wenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 15 za barafu kwa siku na kukaushia zaidi ya kilo 300 za dagaa kwa siku, majokofu 10 yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita 500 kila moja, pamoja na zaidi ya coolbox 20 zenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita 15 kila moja.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Mhe. Prof. Mohammed Sheikh, amesema uwekezaji huo utachochea ongezeko la thamani ya mazao ya uvuvi na kuongeza tija katika sekta hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Mhe. Prof. Mohammed Sheikh, Picha naOfisi ya mawasiliano Kigoma

Aidha, Prof. Sheikh amelishukuru Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kupitia mradi wa FISH4ACP kwa kufanikisha upatikanaji wa mtambo huo, na kuwataka wadau wengine kuendelea kuwekeza katika sekta ya uvuvi ili kukuza uzalishaji.

Miongoni mwa mitambo iliyotolewa kwa ajili ya kuchakata mazao ya uvuvi, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

“Ni muhimu kuongeza uwekezaji katika uzalishaji ili kupunguza uhaba wa mazao ya uvuvi na kukidhi mahitaji ya soko,” amesema Prof. Sheikh.