Joy FM

Wannawake watakiwa kuchangamkia fursa Kasulu

8 June 2026, 14:40

Katibu tawala Wilaya Kasulu, Theresa Mtewele, Picha na Hagai Ruyagila

Katika kuhakikisha wanawake wanajikwamua kiuchumi kutokana na fursa zilizopo kwenye maeneo yao, Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vikundi ili viweze kuendelea kukua na kuwanufaisha wanawake

Na Hagai Riyagila

Wanawake wajasiriamali wa kikundi cha Community Microfinance kinachojishughulisha na ufugaji wa kuku katika Kata ya Muganza, Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, wamesema mradi huo umewasaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha ya familia zao.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa jengo la ufugaji wa kuku la kikundi hicho, Katibu Msaidizi wa Kikundi cha Community Microfinance cha Kata ya Muganza, Berita Barokola, amesema mafanikio yanayopatikana kupitia mradi huo yamechangia kuimarika kwa hali ya uchumi wa wanachama na familia zao.

Wanawake wa kikundi hicho wakionyesha mradi wao kwa Katibu tawala Wilaya Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Godfrey Jeremiah, amesema kikundi hicho ni mfano wa kuigwa kutokana na namna kilivyoweza kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo na kwamba mafanikio ya kikundi hicho yanafungua fursa kwa wananchi wengine kuanzisha na kuendeleza miradi ya uzalishaji mali.

Akizindua jengo hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yao kwa ajili ya maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.