Joy FM
Joy FM
10 June 2026, 16:09

Serikali Wilayani Kakonko Mkoani kigoma imesema inaweendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji ili waweze kuwekeza katika Wilaya hiyo.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa, kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli wamepokea ugeni wa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka kampuni ya Mohammed Enterprises, waliowasili wilayani humo kwa lengo la kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji ili kutathmini fursa zilizopo katika eneo hilo.
Katika mazungumzo yaliyofanyika wilayani Kakonko, viongozi hao wameeleza kuwa wilaya hiyo ina rasilimali na mazingira mazuri yanayoweza kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini, kilimo, biashara, viwanda na huduma za kijamii.

Aidha wamesisitiza utayari wa serikali kushirikiana na sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika maeneo mbalimbali yenye fursa za uwekezaji ikiwemo eneo la Nyamwironge lililopo katika Kijiji cha Nyamtukuza ambapo kuna uchimbaji wa madini ya dhahabu na eneo la Kijiji cha Nyanzige ambapo kuna madini ya chokaa, Kanali Mallasa amesema kuwa Serikali ya Wilaya itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji zaidi, huku akibainisha kuwa uwekezaji ni nguzo muhimu katika kuongeza ajira na kukuza mapato ya wananchi wa Kakonko.

Kwa upande wake, Ndaki Stephano Mhuli, Mkurugenzi mtendaji ameeleza kuwa Halmashauri imejipanga kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kwa kuhakikisha huduma muhimu na taratibu za uwekezaji zinapatikana kwa wakati, jambo litakalosaidia kufungua fursa mpya za maendeleo katika Wilaya hiyo.
Mohd Parvej Ahmad, mmoja wa wakilishi kutoka kampuni ya Mohammed Enterprises alieleza kufurahishwa na fursa alizoziona Kakonko na kubainisha kuwa bado kuna maeneo mengi yenye uwezo mkubwa wa uwekezaji.

Amesema ziara hiyo imewapa nafasi ya kujionea hali halisi ya mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akiahidi kampuni yao kuendelea kuchunguza fursa mbalimbali zitakazoweza kuleta manufaa kwa wananchi na uchumi wa Wilaya na Nchi kwa ujumla.